NA JAMES MUTUA
Wakenya walioshiriki katika utafiti wa TIFA wa hivi karibuni wamempa rais Ruto alama ya C+ kulingana na hisia zao kuhusu ahadi zake za kampeni ya mwaka jana.
Utafiti huo uliotolewa alhamisi katika hoteli moja hapa jijini Nairobi umetoa taswira mbaya ya utendakazi wa serikali ya Kenya Kwanza.
Ripoti ya uchunguzi huo ilifanyika kati ya Juni 24, 2023, na Juni 30, 2023, kwa njia ya mahojiano ya Simu iliyosaidiwa na Kompyuta (CATI) na iliwahusisha wahojiwa 1,530.
Utafiti huo ulihusisha maoni kuhusu mwelekeo wa nchi na utendakazi wa serikali ya Kenya Kwanza tangu ilipochukua hatamu ya uongozi miezi 10 iliyopita. Kulingana na TIFA, idadi kubwa ya Wakenya (56%) wanaamini kuwa nchi inaelekea pabaya.
Ukusanyaji wa takwimu za utafiti ulihitimishwa kabla ya vifungu mbalimbali vya Bajeti mpya kuanza kutumika.
Wakenya wachache wanazingatia mwelekeo wa sasa wa nchi kuwa mzuri (25%), wakiwa na maelezo chache kuhusu sababu zao, huku idadi ndogo ya walio wengi (24%) wakitaja uongozi wa serikali ya Ruto kuwa sababu kuu ya kuwa na msimamo mzuri.
Bila kujali mlengo wao za kisiasa, idadi kubwa ya Wakenya ambao wanaona kuwa nchi inaelekea pabaya, walitaja gharama ya maisha inayoongezeka kila mara.